CHAPO KUZINDUA MAFUNZO MAALUM YA KISHERIA WAWI MACHI 11, 2023
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JUMUIYA ya wasaidizi wa sheria wilaya
ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’, asubuhi ya leo, inatarajia kufungua mafunzo
maalum ya sheria ngazi ya jamii, kwa lengo la kuwapa uwelewa wanajamii.
Akizungumza na
mwandishi wa habari wa hizi ofisini kwake leo Machi 10, 2023 mjini Chake chake, Mkurugenzi wa ‘CHAPO’
Nassor Bilali Ali, alisema, tayari kila kitu kimeshakamilika kuelekea mafunzo
hayo.
Alisema,
mafunzo hayo ya kwanza na maalum kufanywa kwa aina yake, ni miongoni mwa mpango
kazi wa ‘CHAPO’ katika kuwaelimisha wananchi masuala ya kisheria.
Alieleza kuwa,
‘CHAPO’ inaamini kila mwananchi anayo haki ya kupata uwelewa wa masuala ya
kisheria, na ndio maana ‘CHAPO’ ikabuni mpango huo.
Mkurugenzi
huyo alifafanua kuwa, mafunzo hayo kwa kuanzia, yataanzia shehia ya Wawi kama
eneo la majaribio, na kisha kusambaa katika majimbo manne ya wilaya ya Chake
chake.
‘’Uzinduzi
wa mafunzo haya yanatarajiwa kufanyika Machi 11, ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta
ya Makonyo Wawi wilaya ya Chake chake, na tayari kila kitu kimekaa sawa,’’alieleza.
Aidha Mkurugenzi
huyo wa ‘CHAPO’ alisema, ubunifu wa mafunzo hayo, yalitokana na wasaidizi wao
wa sheri wa Jimbo la Wawi, ikiwa ni hatua ya kuwafikia wananchi kupata elimu
hiyo.
‘’Wazo la
wasadizi wa sheria wetu hawa, kwanza tumelipokea mikono miwili, na sasa tumeona
liwe la wilaya nzima, ili kuhakikisha kila jimbo, mafunzo hayo yanasambaa,’’alieleza.
Alieleza kuwa,
kwa hatua za awali jumla ya wananchi 20 wa shehia ya Wawi, wakiwemo wajumbe 10
wa kamati ya sheha na wananchi wengine 10, ndio watakaoingia kwenye mafunzo,’’alifafanua.
Msaidizi wa
sheria Jimbo la Wawi Fatma Hilali, alisema uongozi wa shehia ya Wawi, umeshatoa
baraka zote kuelekea mafunzo hayo, ikiwa ni pamoja na kukubali kutoa washiriki.
Hata hivyo,
alisema anatamani kuona mfumo huo wa mafunzo, unaendelezwa wilaya yote ya Chake
chake na hatimae Zanzibar nzima.
Afisa Sheria
kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Bakari
Omar Ali, alipongeza hatua hiyo, na kuomba zoezi hilo, lihamie kwenye majimbo
na wilaya nyingine.
‘’Ni jukumu
la ‘CHAPO’ na jumuia nyingine kuhakikisha wanawaelimisha wananchi, kutambua
haki na wajibu wao kisheria, ili waishi kwenye bahari ya haki na kuvua samaki
wa uadilifu,’’alieleza.
Hata hivyo,
ameonya kuwa, bado jukumu la kutoa elimu, msaada na ushauri wa kisheria,
utendelea kubakia mikononi mwa wasaidizi wa sheria wanaotambulika kisheria.
Kwenye uzinduzi
wa mafunzo hayo, yanayotarajiwa kuwa ya siku 10, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Afisa Mdhamini wizara ya nchi, afisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi na
Utawala Bora Halima Khamis Ali.
Miongoni mwa
waalikwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Madiwani wilaya ya Chake chake, madiwani wa
wadi za Wara na Kiboni, Mwenyekiti wa masheha, Katibu, Askari shehia na masheha
wa shehia zote zinazounda Jimbo la Wawi.
Mwisho



Comments
Post a Comment