MSAIDIZI WA SHERIA WAWI, AKAGUZWA ARDHI INAYODAIWA KUVAMIWA NA SERIKALI


 

NA MWANDISHI WETU, CHAPO@@@@

MKURUGENZI wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Nassor Bilali Ali, amewataka wamiliki wa ardhi wanaoishi mbali nazo, kujenga utamaduni wa kuzikagua kila, wakati, ili kuepushwa kuvamiwa.

Mkurugenzi huyo aliyasema hayo Machi 24, 2023, eneo Kwasharifuali shehia ya Wawi, wakati akizungumza na walalamikaji wa eneo hilo, walilodai kuvamiwa na Kiwanda cha mafuta ya makonyo zaidi ya miaka sita sasa, kwa shughuli za upandaji wa miti ya biashara.

Alisema, ardhi iliyokaa bila ya kuendelezwa na kisha mmiliki kushindwa kuipitia kila wakati, huwa rahisi mtu yeyote kuanzisha matumizi.

Alieleza kuwa, kama mmiliki anaishi mbali na ardhi husika, ni vyema wakaanzisha uwakala wa ulinzi wa ardhi zao, ili iwe rahisi kupatikana taarifa kwa aina yoyote ile ya matumizi.

Mkurugenzi huyo wa CHAPO alisema, wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu kwa wananchi mbali mbali, juu ya umuhimu wa matumizi ya ardhi.



‘’Wananachi tunawashauri kama wana ardhi ambazo hawajakuwa tayari kuzitumia wao, basi wawape watu wengine kwa maandishi ya mkataba maalum, ili kuepusha wengine kuivamia,’’alieleza.

Katika eneo jingine, alisema ardhi sasa imekugeuka dhahabu kwa kila mmoja, hivyo ni wajibu wa kila mmiliki, kuhakikisha anairasimishi.

‘’Ardhi iliyopimwa, inakuwa na thamani mara mbili, na inaweza kutumika kama kizibiti cha kuombea mkopo katika taasisi mbali mbali za fedha,’’alifafanua.

Akizungumza kwenye ukaguzi huo, Msaidizi wa sheria Jimbo la Wawi Haji Nassor Mohamed, alisema baada ya kupokea malalamiko ya familia Machi 22, 2023, juu ya madai ya kuvamiwa ardhi yao, alifika kwa walalamikiwa.

Alisema kisha Machi 23, 2023 alifika kwa Uongozi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi, pamoja na uongozi wa shehia ya Wawi, juu ya kuwasilisha lalamiko husika.

Kisha uongozi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo, ilipofika Machi 24, ulipenda kukutanishwa na familia inayodai kuvamiwa eneo lao, na baada ya ukaguzi, mazungumzo ya awali yalifanyika.

''Mazungumzo ya awali baina pande mbili hizo, mbele ya Msaidizi wa sheria na sheha wa shehia ya Wawi yalifanyika, ingawa baada ya Kiwanda kudai kuwa wamekodishwa ardhi hiyo, familia inafuatilia Wizara ya Kilimo,''alieleza.

Hata hivyo Msaidizi huyo wa sheria, alisema tokea aanze kazi shehiani humo mwanzoni mwa mwaka huu, migogoro ya ardhi inaonekana kuchukua nafasi, kwani tayari ameshasaidia kufikia mwafaka kwa mgororo wa kuwania mpaka.






Sheha wa shehia ya Wawi Sharifa Waziri Abdalla, alisema alipokea malalamiko hayo, Machi 22, 2023 kwa familia ya Ali Hamad Kheir, ikilalamikia ardhi yao kuvamiwa.

Alisema alifikisha malalamiko hayo kwa uongozi wa Kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi, na kutaka kukutana na wanafamilia, wanaolalamika.

Alisema, amekuwa akipokea migogoro kadhaa ya ardhi, ingawa hatua ya kwanza ni kuzikutanisha pande mbili hizo, na kisha kuangalia, ikiwa sulhu imepatikana.

‘’Kwa sheria zilivyo, wao wenyewe kwanza hutakiwa kufanya mazungumzo ya awali, ikiwa hakuna shida wanaweza kumaliziana,’’alieleza.

Ali Salim Rashid, akizungumza kwa niaba ya familia yake, alisema eneo hilo hadi mwaka 2017, lilikuwa halijavamiwa kuwa kupandwa aina yoyote ya miti.






‘’Lakini kuanzia mwaka 2018, tuliona mmeshapandwa michai chai na mikaratusi, tulipofuatilia tuliambiwa ni mali ya Kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi, na tulianza kufuatilia hapo zamani,’’anasema.

Uongozi wa Kiwanda hicho, ulisema eneo hilo walilipata kutoka mikononi mwa wizara ya Kilimo, na wanalikodi kuanzia mwaka 2001 hadi sasa.

‘’Sisi ardhi hii tumekodishwa na wizara ya Kilimo, tokea mwaka 2001, na tunalipa kila mwaka, hivyo sisi hatujui ilipopatikana, inabidi familia inyolalamika, iende mbele zaidi,’’ulisema uongozi wa Kiwanda.

Kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi, katika eneo la Mtakata lina wastani wa ekari 550, kwa ajili ya shughuli za kilimo cha mchai chai na mikaratusi kwa ajili ya uzalishaji mafuta.

                                Mwisho  

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’