MDHAMINI KATIBA, SHERIA PEMBA AZIITA JUMUIYA NYINGINE KUIGA KWA 'CHAPO'
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
AFISA Mdhamini wizara ya Nchi, Afisi
ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Khamis Ali,
amesema mpango wa kuandaa, darasa la soma la sheria ngazi ya jamii, uliobuniwa
na Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ unafaa
kuigwa na Jumuiya nyingine.
Afisa
Mdhamini huyo, aliyesema hayo ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi wilayani humo,
wakati akiyafungua mafunzo ya siku 10, kisheria kwa wananchi 20 wa shehia ya
Wawi.
Alisema,
CHAPO imeanzisha mpango mzuri, ambao utasiaidia kwa kiasi kikubwa, ile kiu ya
serikali kuu, ya kutaka wananchi wawe na uwelewa wa masuala ya kisheria.
Alieleza kuwa,
pamoja na kwamba Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria ipo kwa kazi, hiyo
lakini ni jambo la faraja kwa Jumuiya ya ‘CHAPO’ kutanua wigo wa elimu ya kisheria.
‘’Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana kwa karibu na skuli ya sheria
Zanzibar, imekuwa ikizalisha wasiaidizi wa sheria, lakini kisha kupanga mpango
kama kuwafikia wananchi, ni nzuri,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, ameitaka CHAPO kuendelea kuwaunganisha wananchi wa wilaya ya Chake
chake, ili kuhakikisha wanashinda vita dhidi ya udhalilishaji, dawa za kulevya,
migogoro ya ardhi na utelekezaji.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema sehemu ya mafunzo hayo,
ni utekelezaji wa mpango kazi wao, ambao unalenga kutoa elimu ya kisheria kwa
jamii.
Hata hivyo,
alisema mafunzo ya siku 10, ni wazo la sheha wa shehi ya Wawi, baada ya kukaa
na wasaidizi wa sheria wao, na kubuni mpango huo.
‘’Ijapokuwa ‘CHAPO’
jukumu lake kubwa ni kutoa elimu, lakini mbinu ya kuanzisha darasa, lazima
tumpongeze sheha wa shehia ya Wawi na hadi kufanikisha, uanzishwaji wa mafunzo
haya,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Mkurugenzi huyo, alisema tayari ‘CHAPO’ tokea kuanzishwa kwake mwaka
2015, imeshawafikia wananchi 24,750 kuwapa elimu pamoja na kufanikiwa kusaidia
moja kwa moja wananchi 430 kupata haki zao.
‘’Ijapo kuwa
sisi wasaidizi wa sheria, katika wilaya ya Chake chake yenye shehia 32, tupo
wastani wa wasaidizi wa sheria 20, lakini kazi tunayofanya ni kubwa,’’alifafanua.
Shehe wa
shehia ya Wawi, Sharifa Ramadhan Abdalla, alisema baada ya kukaa pamoja na
wasaidizi wa sheria aliyokabidhiwa, walibuni uanzishwaji wa mafunzo hayo maalum
ya darasani.
Alisema
mafunzo hayo, yanayotarajiwa kuwa ya siku 10, yameandaliwa kwa pamoja na CHAPO
na wananchi 20 washiriki wa shehia ya Wawi, kutokana na hamu yao kubwa.
‘’Tunahamu
kubwa ya mafunzo ya sheria, ili kwanza yatusaidie sisi, lakini kisha yatatanua
wigo, ili kushirikiana na kufanyakazi kwa karibu na wasaidizi wetu wa sheria,’’alifafanua.
Kaimu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa ‘CHAPO’ Kassim Ali Omar, alisema kama jamii
za shehia nyingine 31 zilizobakia, zitajenga hamu ya kupatiwa mafunzo hayo,
waliowengi watapata uwelewa wa masuala ya kisheria.
Hata hivyo
Kaimu Mwenyekiti huyo, ameitaka ‘CHAPO’ kuendelea na mpango huo kwa shehia
nyingine, ili lengo la wananchi kutambua haki na wajibu wao kisheria, liwe pana
zaidi.
Mwenyekiti
wa masheha wilaya ya Chake chake, Khamis Iddi Songoro, alisema wakati umefika
kwa serikali kuanzisha mfuko wezeshi kwa wasaidizi wa sheria, hasa kutokana na
kazi yao kubwa.
Akiwasilisha
mada ya wajibu na umuhimu wa wasaidizi wa sheria katika jamii, Mwanasheria wa
kujitegemea Khalfan Amour Mohamed, alisema moja ni kupunguza changamoto za kesi
nyingi vituo vya Polisi.
‘’Lakini pia
wasaidizi hawa wa sheria, wanatoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria kwa
jamii bila ya malipo, jambo ambalo ilikuwa kwa malipo hapo zamani,’’alieleza.
Nae Msaidizi
wa sheria Ali Salum, alisema zipo njia mbili kuu za utatuzi wa migogoro,
ikiwemo ya upatanishi na mapatano kwa wanaozozana.
Hata hivyo,
alisema njia hizo kama zikitumika vizuri zinaokoa muda, zinapunguza gharama na
mwafaka wake unadumu.
Wakichangia kwenye
mafunzo hayo, washiriki Fatma Said Juma, Mashavu Juma Mabrouk, Imani Mohamed
Ibrahim, diwani wa wadi wa Wara Kassim Juma Khamis na Juma Mohamed Tamimu,
walisema jambo lililobuniwa na CHAPO ni jema.
Katika mafunzo
hayo ya siku 10, mada kadhaa zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na wajibu wa jamii,
kuzuia dawa za kulevya, njia za utatuzi wa migogoro nje ya mahakama, tofauti ya
kesi na sheria za madai na jinai, mfumo wa mahakama.
Mada
nyingine ni sheria za ardhi, umuhimu wa kurithi kwa kuitumia Kamisheni ya wakfu
na Mali ya Amana, sheria ya Udhahidi, sheria ya Mtoto, njia mbada za malezi ya
watoto pamoja na wajibu wa jamii katika mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Mwisho




.jpg)




.jpg)



Comments
Post a Comment