KAMPENI YA RAIS SAMIA YA 'MSAADA WA KISHERIA' YATAMBULISHW KWA WADAU PEMBA
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
AFISA Mdhamini wizara ya nchi, afisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Utawala bora Pemba, Halima Khamis Ali, amesema kampeni ya kitaifa ya Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan ya msaada wa kisheria, inalenga kutoa ulinzi na upatikanaji haki, kwa wanawake, watoto na wale wa makundi maalum.
Afisa Mdhamini huyo aliyasema hayo Machi 28, 2023, ukumbi wa wizara hiyo Gombani Chake chake Pemba, kwenye mkutano maalum wa kuutambulisha mkakati wa kampeni hiyo, kwa wadau wa haki jinai wakiwemo wasaidizi wa sheria kisiwani humo.
Alisema, kampeni hiyo iliyopewa jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutokana na maono yake ya kwa makundi hayo na mengine, ya upatikanaji wa msaada wa kisheria, kampeni hiyo inakuja kuondoa changamoto hizo.
Alieleza kuwa, kampeni hiyo inagusa kila taasisi katika utekelezaji wake, ikiwemo wasaidizi wa sheria, Jeshi la Polisi, Tume ya haki za bindamu, vyombo vya sheria, Ofisi za ustawi, wizara husika ya katiba na sheria, vyombo vya sheria pamoja na jamii kwa ujumla.
‘’Kampeni hii inataka kuona, zile changamoto za upatikanaji wa msaada wa kisheria na kisha haki kwa wahusika, zinapatikana na hasa kwa wanawake, watoto na wale wenzetu wa makundi maalum,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Afisa Mdhamini huyo alisema eneo jingine katika kampeni hiyo, ni upatikanaji wa wasaidizi wa sheria wapya 5,000 kutoa elimu ya kisheria, kuzisomesha sera na sheria za upatikanaji wa msaada wa kisheria.
Aidha alisema, kila mdau kama ataitekeleza ipasavyo kampeni hiyo, majibu ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan, yatafikiwa.
Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Ali Haji Hassan, alisema ujio wa kampeni hiyo, ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati, wa utoaji wa msaada wa kisheria Tanzania.
Alieleza kuwa, kampeni ambayo ni kwa ajili ya Tanzania bara na Zanzibar, imekuja ili kuimarisha upatikanaji wa msaada wa kisheria, kwa wananchi hasa wasiokuwa na uwezo.
‘’Tunaelewa kuwa zipo sheria kama ile ya Msaada wa Kisheria Tanzania bara, nambari 1 ya Mwaka 2017, Kanuni zake za mwaka 2018 na sheria nambari 13 ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019 kwa upande wa Zanzibar, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambazo ndio msingi mkuu wa utoaji wa msaada wa kisheria,’’alieleza.
Akiwasilisha mpango wa mkakati wa kampeni hiyo, Afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Yussfa Abdalla Said, alisema kila mmoja kwa nafasi yake ni mtekelezaji wa kampeni hiyo.
Alifahamisha kuwa, utekelezaji wa kampeni hiyo unatarajia kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii, hususan haki za wanawake na watoto.
Alieleza kuwa jengine ni kuimarisha huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa huduma za kisheria.
‘’Kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu elimu ya sheria kwa umma, masuala ya haki na wajibu na misingi ya utawala bora, na kuwa na huduma endelevu za msaada wa kisheria katika ngazi zote za kijamii,’’alifafanua Afisa huyo.
Wakichangia, baada ya uwasilishwaji wa kampeni hiyo, washiriki akiwemo, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani Nassor Hakim Haji, alisema kampeni hiyo, inaweza kufungua ufahamu kwa Jeshi la Polisi.
‘’Hadi leo bado baadhi ya vituo vya Jeshi la Polisi, wanawazuia watuhumiwa zaidi ya muda wa kisheria, inakuwa kila siku uende kuuliza sababu hizo, sasa kampeni hii itawazindua,’’alieleza.
Nae mjumbe kutoka Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ‘JUMAZA’ Nassor Abdalla Mauli, alisema kampeni hiyo ni nzuri, ikiwa jamii na wadau, wataweka kando siasa zao.
Msadizi wa sheria Jimbo la Chake chake Mashavu Juma Mabrouk na Mratibu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Pemba, Suleiman Salim walisema kazi iliyobakia ni wananchi, kuelimishwa juu ya mpango huo.
Wakati huo huo Afisa sheria wa Idara hiyo Pemba, Bakar Omar Ali, alisema wanasiasa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo, ingawa hakuwashirikisha moja kwa moja.
‘’Ni kweli wanasiasa ni jukwaa muhimu katika kampeni hii, lakini wanaweza kushiriki, ingawa sio moja kwa moja, kama walivyo wadau wengine,’’alifafanua.
Kampeni hiyo ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ilizinduliwa Machi 1, mwaka huu na ikitarajiwa kumalizika Machi 2026.
Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inalenga kulinda na kukuza haki ya upatikanaji haki kupitia huduma za msaada wa kisheria nchini.
Kampeni hii inatarajia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.
Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa.
Utekelezaji wa kampeni hii, unatarajia kuongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto.
Aidha kampeni hii inatarajiwa kuimarisha huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia.
Jengine ni kuwa, maono ya mabadiliko ya huduma ya msaada wa kisheria umetokana na azma ya Dk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha mfumo wa kutatua changamoto zinazowakumba wananchi bila kusubiria wananchi kuwasilisha changamoto zao wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa.
Ambapo kampeni hiyo ya msaada wa kisheria itaongozwa na kauli mbiu isemayo Msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo”
Mwisho







Comments
Post a Comment