MWAKILISHI WAWI ABARIKI CHAPO KUANZISHA DARASA LA SHERIA KWA WANANCHI

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA::

MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, ameunga mkono, wazo la wasaidizi wa sheria Jimbo la Wawi, la kutaka kuanzishwa darasa maalum la kutoa elimu ya sheria, kwa wananchi wa shehia ya Wawi jimboni humo.

Alisema, wazo la wasaidizi hao wa sheria, kutaka kuanzisha darasa maalum, ni jambo la msingi, kwani elimu waliyopatiwa wao, itasambaa kwa upana.

Mwakilishi huyo aliyasema hayo, Febuari 19, 2023 wakati akizungumza na uongozi wa shehia ya Wawi, kwenye kikao maalum cha maandalizi ya darasa hilo.

Alisema, wananchi wanahitaji kupata elimu ya kujua haki na wajibu wao kwa jamii, samba mba na kupata uwelewa wa mambo ya kisheria.

‘’Kwanza niunge mkono wazo ambalo wenzetu hawa wasaidizi wa sheria Jimbo la Wawi, wameliwaza na mimi nitaunga mkono kwa hali na mali, ili kufanikisha darasa hilo,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Mwakilishi huyo wa Jimbo la Wawi aliwataka wasaidizi hao wa sheria, kuhakikisha darasa hilo linakuwa endelevu, kwa kundi jingine hapo baadae.

Kwa upande wake Sheha wa shehia ya Wawi Sharifa Waziri, alisema amelipokea wazo hilo la kuanzisha darasa maalum la elimu ya sheria, kutoka kwa wasaidizi wa sheria jimboni humo.

‘’Tayari tumeshawateua vijana 10 ambao wataungana na wajumbe tisa wa shehia, katika darasa hilo ambalo linatarajiwa kuanza mwezi ujao,’’alieleza.

Hata hivyo sheha huyo alisema, atahakikisha darasa hilo linakuwa endelevu, ili makundi mengine ndani ya shehia hiyo, yaweza kufaidika na elimu hiyo.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema wameamua kuanzisha darasa hilo, ili elimu ya sheria ifike kwa upana kwa jamii.



‘’Mikutano yetu ya kila shehia ya kukutana na makundi mbali mbali ya jamii kuwaelimisha juu ya mambo ya udhalilishaji, dawa za kulevya na migogoro ya ardhi, ipo kama kawaida,’’alieleza.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema, gharama za uendeshaji wa mafunzo hayo yanayotarajiwa kuwa ya siku 10, zitabebwa na ‘CHAPO’ kwa kushirikiana na wadau wengine, ili kuhakikisha jamii, inapata elimu.

Hata hivyo alisema darasa hilo litakuwa kwa wilaya nzima, ingawa kwa kuanzia litaanzia shehia ya Wawi Jimbo la Wawi, kama eneo la majaribio.

Kwa upande wake Msaidizi wa sheria wa jimboni humo Fatma Hilali, alisema baada ya kufikiria waliona ni vyema sasa kuzaa wazo hilo, ili kuhakikisha elimu inasambaa.

‘’Tuliona tuanzishe darasa maalum, ambalo litakuwa na wananchi 20 kwa hatua za awali, ili kuwa nao darasani, kwa lengo la kuwasomesha sheria,’’alieleza.



Mmoja kati wanafunzi tarajiwa kwenye darasa hilo Issa Omar, alisema watahakikisha wanashiriki vyema kwenye darasa hilo, mwanzo hadi mwisho.

Nae Afua Ali Hamad, alisema wamefurahishwa mno na uamuzi wa wasaidizi wao wa sheria wa kuanzisha darasa maalum.

                            Mwisho    

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’