WANAFUNZI WA MADRASSA CHAKE CHAKE WAONESHWA NJIA KUJIKINGA NA UDHALILISHAJI
NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
IDARA ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, ofisi ya Pemba, imewakumbusha wanafunzi wa madrassa za qur-an kisiwani Pemba, kujitenga mbali na watu wanaowanesha dalili za vitendo vya udhalilishaji, ikiwa ni pamoja na kuwawekea picha chafu kupitia simu zao.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari, 7 2023 kwa nyakati tofauti, na mwakilishi wa Idara hiyo Mohamed Massoud Said, wakati akizungumza na wanafunzi wa madarassa za Vikunguni na Machomane wilaya ya Chake chake, kwenye ziara maalum, ya kutoa elimu ya kupambana na matendo hayo.
Alisema, moja ya dalili ya mtu anaetaka kumdhalilisha mtoto huanza kwa kumuonesha picha za ngono, kumnunulia zawadi, kumpa fedha, na kuendelea kwa maneno ya ushawishi juu ya udhalilishaji.
Alisema ni jukumu lao, kwanza kutoshirikiana na watu wa aina hiyo, hata ikiwa ni wazazi wao, au kutoa taarifa kwa watu wengine, kabla ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Mwakilishi huyo wa Idara ya Katiba na msaada wa kisheria, aliwataka wanafunzi, pamoja na kujitenga na watu wa aina hiyo, lakini wasisite kuwatangaaza juu ya nia yao ovu.
‘’Wanafunzi mjue kuwa, wanaotaka kuwadhalilisha wana njia nyingi, moja wapo ni kuwapa zawadi, pesa au kuwaonesha picha za vitendo vichafu, kama njia ya kuwarubuni kabla ya kuwadhalilisha,’’alisema.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi, waalimu, wazazi na walezi kuitumia Idara hiyo kwa kutoa taarifa za matukio hayo, au uwepo wa watu wanaojaribu, kuzifanyia sulhu kesi za udhalilishaji.
Mkurugenzi wa Jumuiya wa wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, amesema kama jamii haikushirikiana katika ulinzi wa watoto, kusitarajiwe matendo hayo kupungua.
Alieleza kuwa, watoto ni rasilimali ya taifa, hivyo kama jamii ya sasa haikuchukua tahadhari ya kuwalinda, inaweza kuwa vigumu hapo baadae, kupata viongozi na waalimu bora.
Alisema, kama wazazi wanatabia ya kutoshiriki vikao vinavyoitwishwa na waalimu, inaweza kuwa vigumu, kuwalinda watoto waalimu peke yao.
Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, aliwataka wanafunzi hao, kutomruhusu mtu yeyote, kuuchezea mwili wake.
‘’Sehemu zako za siri ni mali yako, usimuonesha mtu mwengine wala usikubali kuguswa kama hakuna sababu inayokubalika, maana huo ndio mwanzo, wa udhalilishaji unapoanzia,’’alieleza.
Mratibu wa Idara ya watu wenye ulemavu Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, ameitaka jamii, kuwatoa ndani watoto wenye ulemavu, ili kupata haki yao masingi kama elimu.
Hata hivyo amesema, lazima ulinzi kwa watu wenye ulemavu uimarishwe mara mbili, ili wawe huru na matendao ya udhalilishaji wa kijinsia, yaliokithiri.
‘’Watoto wote wanapaswa walindwe dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ingawa hawa wenzetu wenye ulemavu, wanatakiwa juhudi iongezwe, kutokana na mazingira yao,’’alifafanua.
Mwalimu mkuu wa almadrassatul-Annajah Imani Ali Mohamed, alisema ziara hiyo kwao ni faraja, katika kuwakumbusha wanafunzi na matendo hayo.
Kwa upande wake Msaidizi mwalimu mkuu wa almadrassatul-Umi ya Vikunguni Zubeda Yussuf Mohamed, alisema bado wazazi hawajaona umuhimu wa kushirikiana na waalimu, katika malezi ya watoto.
Baadhi ya wanafunzi wa madrassa hizo, walisema elimu walioipata, imewasadia katika kujikinga na matendo ya ukatili na udhalilishaji.
Hata hivyo walisema, bado adhabu kali kwa wakosaji haijatolewa mahakamani, na ndio maana makosa hayo, yamekuwa yakijitokeza, kila siku ndani ya jamii.
Zira hiyo ya kutoa elimu ya kupambana na makosa ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, ni muendelezo ya mikakati ya Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, katika kuhakikisha kundi la wanawake na watoto, linaishi pasi na ukatili.
Ripoti ya Jeshi la Polisi Zanzibar, inaonesha, kwa mwaka 2021, kulikuwa na matendo 1,222 ya wanawake na watoto kudhalilishwa Unguja na Pemba.
Aidha ripoti nyingine ikaonesha kuwa, kulikuwa na matukio 610 ya aina hiyo, kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu ya mwaka 2021 na 2022.
Kwa miezi ya Januari hadi Machi mwaka 2021, Jeshi la Polisi Zanzibar, lilikusanya matukio 363, ingawa kwa mwaka jana katika kipindi kama hicho, yaliripotiwa matukio 247, upunguzu wa matukio 116.
Takwimu hizo zinafafanua kuwa, kwa mwaka 2021 kwa miezi mitatu ya mwanzo, mwezi ulioongoza ni Machi, ulioripoti matukio 141, ukifuatiwa na Januari 122 na Febuari matukio 100.
Kwa mwaka 2022, mwezi uliokihiri kwa matukio ni mwezi Febuari matukio 100, mwezi Machi matukio 82, wakati mwezi wa Januari yakishuka kwa 17, na kuripotiwa matukio 65.
Taarifa hiyo ikeleza kuwa, mwezi wa Febuari kwa miaka yote miwili, iliripoti matukio sawa ya 100 kwa wanawake na watoto kudhalilishwa kwa Unguja na Pemba.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba Juma Saad Khamis, alisema moja ya vyanzo vya matukio hayo, ni mporomoko wa maadili, uliozoeleka ndani ya jamii.
Hakimu wa mahakama amaalum ya kupambana na makosa ya udhalilishaji mkoa wa kusini Pemba Muumini Ali Juma, alisema chanzo ni wazazi kuacha malezi ya pamoja.
Mwanasheria dhamana wa Mahakama kuu Zanzibar Ali Rajab, anasema kuongezeka kwa matukio hayo, ni jamii kukosa elimu ya kisaikolojia, na kuyapa uzito matukio hayo yapotokezea.
Mzazi Saumu Haji Said wa Machomane anasema, kutotumika kwa sheria kama zilivyoandikwa, baada ya mtuhumiwa wa udhalilishaji kutiwa hatiani, ndio sababu ya kuongezeka.
Daktari Mohamed Ali Jape anasema, kupoteza haiba ya viungo vya mwili, ndio athari kubwa inayowaumiza watoto hasa kutokana na umri wao kutokuwa tayari kufanya tendo hilo.
Mwisho
.jpg)










Comments
Post a Comment