MDHAMINI KATIBA, SHERIA: 'AWAPA TANO WASAIDIZI WA SHERIA PEMBA'

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA::

AFISA Mdhamini wizara ya nchi afisi ya rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba Halima Khamis Ali, amesema kazi inayofanywa na wasaidizi wa sheria na watoa msaada wa kisheria, imesaidia kuonesha jamii njia ya haki na kuacha batili.

Afisa Mdhamini huyo aliyaeleza hayo, ukumbi wa wizara hiyo, kwenye mkutano wa robo mwaka, wa masuala ya msaada wa kisheria, ulioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar.

Alisema, licha ya changamoto kadhaa walizonazo watoa na wasaidizi hao wa msaada wa kisheria hao, lakini kwa sasa hali inaridhisha ya wananchi, kuzijua haki zao mbali mbali.

Alieleza kuwa, jamii awali haikuwa na uwelewa mpana wa haki zao mbali mbali, lakini baada ya Idara ya Katiba na Msaada wa sheria kuwajengea uwezo na kisha kwenda mtaani, hali inaridhisha.

‘’Kwa haki bado msingi mkuu kwa jamii kuzipata na kuzijua haki zao zitabakia kuwa, zimeimarisha na watoa na wasaidizi wa sheria waliomo shehiani, kwa hili hongereni,’’alifafanua.



Katika hatua nyingine, Afisa Mdhamini huyo, amewataka wasaidizi hao wa sheria, kuyafanyiakazi maazimio wanayokubaliana, katika vikao kama hivyo.

‘’Moja ya jambo ambalo kwenye mkutano wa mwaka jana mlilipitisha ni nyinyi kupata mafunzo ya upigaji picha, mafunzo ya lugha za alama, lakini mmeshindwa kufanikisha kwa sababu nyepesi,’’alieleza.

Mapema akizungumza kwenye mkutano huo, Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Ali Haji Hassan, alisema bado jitihada zinahitajika kwa wasaidizi wa sheria, katika kuifikia jamii.



Hata hivyo amewakumbusha watoa msaada hao na viongozi wa jumuiya ya wasaidizi wa sheria, kuwakumbusha wanachama wao kujisajili, kwani kinyume chake, kisheria hawezi kuihudumia jamii.

‘’Sheria yetu inatuongoza kuwa, kila mwaka tufanya usajili na hili ni takwa la kisheria, na kinyume chake Idara na hata hizo Jumuiya itakuwa hazitambui uwepo wenu,’’alieleza.

Akiwasilisha tathmini ya jukwaa la pili la mwaka la msaada wa kisheria Zanzibar, Afisa huyo alisema mengi yamejitokeza, ikiwa ni pamoja na wazo la kuundwa mfuko wa wasaidizi wa sheria.

Alisema, jengine ni kuendelea kujengewa uwezo wasaidizi wa sheria, ili kuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi, ili kutimiza malengo yao.





Akiwasilisha ripoti ya utendaji, Mkurugenzi wa Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema wamekuwa wakishirikiana na taasisi mbali mbali, katika kuwafikia wananchi.

‘’Tumekuwa tukishirikiana na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’, TAMWA-Zanzibar, TUJIPE, na jumuiya nyingine za wasaidizi wa sheria kisiwani Pemba,’’alieleza.





Nae Mkurugenzi wa wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani ‘MDIPAU’ Nassor Hakim Haji, alisema changamoto kubwa wanayoiona na jamii, kutokuwa tayari kuhudhuria kwenye vikao vyao.

Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, imekuwa ikiendesha mafunzo, makongamano na majukwaa kwa wasaidizi wa sheria na watoa msaada wa kisheria, ili kuwajengea uwezo katika kazi zao.

                             Mwisho

  

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’