IDARA KATIBA SHERIA YAUKARIBISHA MWAKA MPYA, YASEMA JAMBO MATUKIO YA UDHALILISHAJI

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA::

WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa kuufanya mwaka mpya wa 2023, uwe wa mageuzi kwa kupunguza matukio ya ukatili na udhalilishaji, kwa kuwatumia wasaidizi wa sheria, ili kupata elimu, ushauri na msaada wa kisheria.

 

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 5, 2023 na Afisa sheria, kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, ofisi ya Pemba Bakari Omar Ali, wakati akizungumza na mwandishi hizi, katika kuukaribisha mwaka mpya.

 

Alisema, matukio ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto bado yalikuwa yameshika kasi kwa mwaka 2022, hivyo amewataka wananchi, kwa mwaka huu 2023 uwe mwaka wa mageuzi kwa kupunguza matukio hayo.

 

Alieleza kuwa, Idara inaowasaidizi wa sheria katika kila jimbo la uchaguzi, hivyo ni vyema wakawatumia ili kupata uwelewa wa kisheria, sambamba na elimu ya kupambana na matukio hayo.

 

Afisa sheria huyo alifafanua kuwa, wasadizi hao wa sheria, wako tayari na saa yoyote kutoa elimu na msaada wa kisheria, bila ya malipo, hivyo ni wajibu wa wananchi, kuwa nao karibu.

 

‘’Zanzibar bila ya kuwa na matendo ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto inawezekana sana, ikiwa jamii itafanyakazi kazi, kwa karibu na wasaidizi wa sheria,’’alieleza.

 

Katika hatua nyingine Afisa sheria huyo, amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya sheria, kama jeshi la Polisi, Mahakama katika kutokomeza matendo hayo.

 


Alisema moja ya changamoto iliyojitokeza kwa mwaka uliomalizika, ni kwa wananchi, kutofika mahakamani kutoa ushahidi na kusababisha kesi nyingine kuondolewa.

 

‘’Wapo watuhumiwa kadhaa wa makosa ya ukatili na udhalilishaji kwa mwaka jana, wameachiwa huru, baada ya mashuhuda wa matukio hayo, kukataa kufika mahakamani kutoa ushahidi,’’alisema.

 

Wakati huo huo, Afisa huyo amezitaka jumuia za wasaidizi wa sheria Pemba, kuendelea kuwa karibu na Idara hiyo, ili kufanikisha majukumu yake mbali mbali.

 


Alisema kwa mwaka uliopita, walishirikiana vyema na Idara hiyo, hali iliyopelekea kufanikisha shughuli mbali mbali, kama mikutano ya wazi ya utoaji elimu ya kisheria.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jumuia ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, aliipongeza Idara hiyo, kwa kuendelea kuwaamini katika utendaji wao wa kazi.

 

‘’Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, imekua ikituamini katika utendaji wetu wa kazi, na tunashirikiana kwa karibu, katika kufanikisha azma ya kuwafikia wananchi,’’alieleza.

 

Hivyo Mkurugenzi huyo, ameuhakikisha uongozi wa Idara hiyo kuwa, kwa mwaka huu wa 2023, watazidisha kasi na kufanyakazi kwa karibu, ili wananchi wazitambue haki zao.

 

Nae Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria Mkoani Nassor Hakim Haji, aliipongeza Idara hiyo, kuwa kufanikisha jukwaa la pili la msaada wa kisheria, lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana kisiwani Unguja.

 



Hata hivyo amewakumbusha watendaji wenzake, kuzidisha kasi, ari na hamu ya kuwahudumia wananchi, katika kupambana na matendo ya dawa za kulevya na udhalilishaji.

 

Akizungumza hivi karibuni, kwenye jukwaa la pili la msaada wa kisheria, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Hanifa Ramadhan Said, alisema mwaka 2023, utakuwa mzuri kama ushirikiano utaongezeka.

 

‘’Mimi najua kwenye jumuia za wasaidizi wa sheria, zipo changamoto mfano gharama za kukodi za ofisi, ukosefu wa usafiri, lakini tuongeze juhudi za kuwafikia wananchi popote walipo,’’alishauri.

 


Baadhi ya wananchi kisiwani Pemba, walisema kazi inayofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwa kushirikiana na wasaidizi wa sheria ni kubwa, ingawa kwa mwaka huu, lazima ushirikiano wao uongezeke.

 

Mnufaika wa msaada wa kisheria kutoka shehia ya Madungu wilaya ya Chake chake, Asha Hussein Seif, anasema upo umuhimu mkubwa wa wasaidizi wa sheria, kuendelea kujengewa uwezo.

                              Mwisho    

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’