CHAPO: WASAIDIZI WAPYA WA SHERIA MASHEHA NDIO WENYEJI WENU SHEHIANI
NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
WASAIDIZI
wapya wa sheria wa majimbo ya wilaya ya Chake chake kisiwani Pemba, wametakiwa
kushirikiana na masheha kwenye shehia zao, ikiwa wanata kufanikiwa katika kazi
zao, za utoaji elimu, msaada na ushauri wa kisheria kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 27, 2023 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Safia
Saleh Sultan, wakati akizungumza na wasaidizi hao, ofisini hapo mjini Chake
chake.
Alisema, kila msaidizi wa sheria, mwenzake katika
shehia yoyote ile ni Sheha wa shehia husika, kwani ndie mwenyeji wake kikazi,
na si vyema kumdharau.
Alieleza kuwa, kazi ya msaidizi wa sheria moja ya
wajibu wake, ni kuhakikisha anafanyakazi bega kwa bega na sheha au wajumbe wa
sheha, ili kufanikisha kazi zao zake.
‘’Mnakwenda kwenye shehia, lakini muelewe kuwa,
msishahu kuwa Sheha ndio mwenyeji wako, na usijaribu kufanya jambo lolote, pasi
na kumuomba ruhusa,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya
CHAPO, alifahamisha kuwa, ushirikiano baina ya wasaidizi hao wa sheria wapya na
wale wakongwe, ni jambo la muhimu.
‘’Sote tunajenga nyumba moja ya kuisaisdia jamii yetu,
sasa hakuna huja ya mivutano, bali ili mufanikiwe mujenge
ushirikiano,’’alieleza.
Hata hivyo ameutaka uongozi wa CHAPO, kuendelea
kukutana na wasaidizi hao wa sheria kila wakati, hasa kipindi hiki wakiwa bado
wachanga katika kazi hiyo.
Kwa upande Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali,
alisema kwa vile wasaidizi hao wapya wa sheria wameshajisajili na kutambulika,
kazi iliyoko mbele yao sasa ni kuihudumia jamii.
Aliongeza kuwa, moja ya majukumu ya msaidizi wa sheria
ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria kwa watu wasio na uwezo, tena
bila ya malipo.
‘’Mukumbuke kuwa, moja ya kazi zenu ni kutoa elimu, na
msaada wa kisheria tena bila ya malipo, maana kazi hii, zaidi msingi wake ni
kujitolea,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa CHAPO, alisisitiza
haja kwa wasaidizi hao wa sheria, kuendelea kujifunza kwa kusoma machapisho
mbali mbali ya kisheria.
Msaisdizi wa sheria jimbo la Chonga Juma Seif Haji,
alisema atahakikisha anashirikiana na sheha na wasaidizi wa sheria
waliomtangulia, ili kufanikisha azma ya kuwahudhumia wananchi.
Nae msaidizi wa sheria Jimbo la Chake chake, Wahida
Kombo Khamis alisema kazi hiyo inahitaji umakini mkubwa, ili kuhakikisha jamii
haiyumbi.
Wasaidizi hao wa sheria wapya, tayari wameshakamilisha
usajili chini ya Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria pamoja na kujiunga na
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake Chake ‘CHAPO’.
Mwisho






Comments
Post a Comment