MSAIDIZI WA SHERIA WESHA AWAPA MBINU WANAWAKE MALEZI YA WATOTO
NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
WANAWAKE
wa kijiji cha Kaole, shehia ya Wesha wilaya ya Chake chake Pemba, wametakiwa
kujitathimini aina ya malezi wanayowarithisha watoto wao, ikiwa ni mwafaka, kwa
ajili ya kuyamudu mazingira yao, ya kupambana na majanga mbali mbali, kama ya
ukatili na udhalilishaji.
Ushauri huo umetolewa Novemba 5, mwaka 2022 na Msaidizi wa sheria wa shehia za Wesha na Ndagoni wilayani humo, Khadija Said
Khalfan wakati akizungumza na wananchi hao, kwenye mkutano wa wazi wa kutoa
elimu, ndani ya siku 16 za kupinga ukatili, mkutano ulioandaliwa na Jamuiya ya
wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’.
Alisema, kila utafiti
unaofanywa, umekuwa ukiwaangukia wanawake, kuwa wamelengaza kamba katika malezi,
na wapo baadhi yao, wamekuwa wakiwarithisha malezi mabovu watoto wao.
Alieleza kuwa, kwa mfano
wapo wanawake wamekuwa wakiwafichia uovu hasa watoto wa kike, na kujenga uadui
kwa baba yao, jambo ambalo halimsaidii mtoto, katika maisha yake ya baadae.
‘’Utamskia mama ataka
kumrushu mtoto wake kwenda atakako, ingawa anamueleza kuwa baba yake ndio kikwazo,’’huu
sio utamaduni mzuri katika malezi.
Aidha msaidizi huyo wa
sheria, katika shehia za Wesha na Ndagoni, Khadija Said Khalfan alisema, malezi
mengine ambayo sio mwafaka kwa maendeleo ya mtoto, ni wazazi walio wengi kuwaachia
simu watoto wao.
‘’Sasa walezi wakubwa kwa
sisi wanawake ni kumfungulia simu mtoto wakati anapolia, aina ya picha na
muziki wanaowekewa anajua mama mwenyewe,’’alifafanua.
Akizungumzia vitendo vya
ukatili na udhalilishaji, alisema namna ya kuviondoa, ni jamii kushirikiana kwa
dhati na vyombo vya ulinzi na vya sheria.
‘’Njia nyingine, ambayo ni
rahisi katika kutokomeza matendo haya, ni kufika mahakamani kutoa ushahidi, kupambana
na kushirikiana katika malezi, kati ya baba na mama,’’alifafanua.
Hata hivyo amewataka
wananchi hao, kuitumia ofisi yao CHAPO, wanapohisi wamewakosa wasaidizi wa
sheria waliomo shehiani mwao, ambapo watapewa elimu, ushauri na msaada wa
kisheria bila ya malipo.
Akifungua mkutano huo Sheha
wa shehia ya Wesha, Haji Mohamed Ali, alisema kazi inayofanywa na wasaidizi wa
sheria ni kubwa, na kilichobaki kwa wananchi, ni kubadilika kivitendo.
‘’Katika tasisi inayoongoza
kwa kuwafikia wananchi, ni wasaidizi wa sheria kutoka ‘CHAPO’ na naamini, kila
mwananchi anaefika kwenye mikutano yao, anapa elimu ya kupambana na vitendo
hivyo,’’alieleza.
Akiwasilisha mada ya njia ya
kutokomeza matendo hayo, msaidizi wa sheria kutoka Jimbo la Chake chake, Wahida
Kombo Khamis, alisema ni jamii kuyachukia kwa vitendo.
Njia nyingine, alisema ni
kurudi katika imaani za kidini, ambapo hakuna hata dini moja, inayoruhusu
matendo hayo, bali ni mtu mwenyewe tu kwa kule kukosa maadili.
‘’Mimi niwashauri, kama nia
ya kutokomeza matendo haya ipo, basi kwanza tuanze kwa ngazi ya kijiji,
kuyarejesha yale malezi ya zamani, ambayo mtoto mmoja akilelewa na watu
wote,’’alishauri.
Baadhi wananchi wa kijiji
hicho, akiwemo Raya Khamis Abdalla, alisema dhabu nyepesi kwa wanaotiwa hatiani
kwa makosa ya udhalilishaji, bado haijawatia woga wengine.
‘’Mpaka leo unaskia kwenye
vyombo vya habari kuwa, mshitakiwa wa ubakaji, amefungwa miaka saba, 10 na 20,
wakati sheria, tunaambiwa inaekeleza miaka 30 au kifungo cha maisha,’’alisema.
Nae Maryam Said Sabour,
alisema kama jamii haikushirikiana katika mapambano hayo, itakuwa ndoto
kuondoka kwake, maana watendaji wa matukio hayo, wanatoka katika jamii.
Kwa upande wao Ali Ghalib
Omar, Khamis Said Hamad na Asha Said Ali, walisema bado harufu ya rushwa kwenye
vyombo vya sheria, inanukia.
Mapema askari kutoka kituo
cha Polisi wilaya ya Chake chake anayeshughulikia shehia ya Wesha Khamis Ali
Khamis, alisema jamii, ikiamua kupambana na uhalifu, shehia itakuwa salama.
Mkutano huo wa wazi shehia
ya Wesha, ni muendelezo wa mikutano inayofanywa na ‘CHAPO’ katika siku hizi 16
za kupinga ukatili, ambapo shehia za Ole, Ndagoni, Ziwani tayari mikutano kama huo.
Mwisho

















Comments
Post a Comment