MKURUGENZI 'CHAPO' AONA MBALI KWA WASAIDIZI WA SHERIA
NA HAJI
NASSOR, PEMBA
MKURUGENZI
wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor
Bilali Ali, amesema wakati umefika sasa, kwa sheria ya Msaada wa kisheria
Zanzibar, kuweka kipengele cha kuwaruhusu wasaidizi wa sheria, kuingia
mahakamani kuwawakilisha wateja wao.
Alisema, kwa elimu yao inafaa sana sheria iwaruhusu kuingia mahakama za
mwanzo na wilaya, ili wanapokuwa na kesi za mwananchi, na ikifikia wakati wa
kwenda mahakamani, sheria iwaruhusu.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo Disemba 19, 2022, kwenye mkutano kwa njia ya zoom wa
kuwasilisha utafiti wa awali, wa haki ya mwanamke kumiliki mali, uliofanywa Tanzania
bara na Zanzibar, kupitia tasisi ya LSF.
Alisema, wakati mwengine wasaidizi wa sheria wamekuwa wakiianza na
kuendeleza vyema kesi husika, lakini hukorogeka na mwananchi kukosa haki yake,
kwa kule kushindwa kujieleza mahakamani.
Alieleza kuwa, wakati mwengine sio kila lalamiko mfano la ardhi,
huduma, madeni linaiishia mikononi mwa wasaidizi wa sheria, bali mengine hufika
hadi mahakamani.
‘’Mimi nipendekeze kuwa, sasa wakati umefika kwa wasaidizi wa sheria,
kuruhusiwa kuingia mahakamani, ili kumuwakilisha mwananchi au wananchi, mwenye
lalamiko fulani,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo, aliipongeza tasisi ya LSF kwa
kufadhili utafiti huo, ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia kujua kiwango chao
cha kutoa msaada wa kisheria.
Aidha alifahamisha kuwa, pamoja na kwamba uatafiti huo haujaanza
kusambaazwa rasmi, hivyo wakati ukifika wa kuwekwa hadharani, utawasaidia wadau
wengine wa haki za wanawake.
Akiwasilisha utafiti huo wa awali, Mhdhiri kutoka Chuo cha Mzumbe, Dk.
Lukiko Lukiko, alisema changamoto bado ipo inayowakabili wanawake, katika
umikili wa rasilimali.
Alieleza kuwa, wamegundua kuwa wapo baadhi ya wanaume wamekuwa wakivaa
majoho ya ubepari, dhulma hali inayopelekea wanawake, kukosa kumiliki mali.
‘’Ijapokuwa utafiti huu, kisha utawekwa hadharani na hasa baada ya
mawasilisho haya ya awali, ambayo pia yatongeza jambo, lakini hali inaonesha ni
mbaya,’’alieleza.
Nae mdau John Ngiga alisema, jambo lililofanywa na LFS ni jema, na
litawapa elimu mpya juu ya umiliki, changamoto kwa wanawake katika kumilika
mali.
Kwa upande wake, Imakulate Mwigani, alieleza kuwa kazi inayofanywa na
LSF inafaa kuungwa mkono na kila mmoja, ili kuhakikisha kundi la wanawake na
watoto linapata haki zao.
Kwa upande mwengine, Afisa wa sheria kutoka
Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba, Bakar Omar Ali,
alisema kwa sasa sheria ya Msaada wa Kisheria Zanzibar nambari 13 ya mwaka 2018, iko kimnya juu ya jambo hilo.
Hata hivyo alisema, msaidizi wa sheria anaweza kuingia mahakamani kama
wakala, ikiwa anataka kumuwakilisha mtu kwenye mahakama.
Mwisho


Comments
Post a Comment