KONGAMANO SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI, WATOTO MIAKA 14 HADI 17 PASUA KICHWA

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA:::

MAHAKAMA maalum ya kupamba na makosa ya ukatili na udhalilishaji mkoa wa kusini Pemba, imesema kesi za udhalilishaji zinazowahusu watoto wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 17, ndio pekee zinazowatesa wao na ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, kwa kule kukataa kutoa ushahidi.

Kauli hiyo, imetolewa Novemba 2, mwaka 2022 na Hakimu wa mahakama hiyo Muumini Ali Juma, wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya masuali yalioulizwa na wananchi, kwenye kongamano la kuelekea siku 16 za kupinga ukatili, lililofanyika Kiwanda cha Makonyo Wawi.

Alisema, mara matukio hayo yanapotekezea kwenye jamii, wazazi wao huwa na ari, kasi na hamu ya kuyafikisha mbele ya vyombo vya sheria, ingawa baada ya muda, hawaonekani mahakamani.

Alisema, na hasa kesi za aina hiyo zinazowaweka njia panda ni zile zinazowakabili watoto wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17, ambao kimatendo ni watu wazima.

‘’Hao wanaobahatika kufika mahakamani, basi wakati wa kutoa ushahidi hueleza kuwa, wale watuhumiwa waliodai kuwabaka hawawajui, na kuiacha njia panda mahakama na upande wa mashtaka,’’alisema.



Aidha Hakimu huyo alisema, suala la kufika mahakamani kutoa  ushahidi, ni njia moja muhimu na ya haraka katika kuyapunguza ama kuyaondoa matendo hayo.

Akifungua kongamano hilo, Msaidizi Kamishna wa Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba Cyprian Mushi, alisema kila mmoja akitekeleza wajibu wake, matendo hayo yatakoma.

‘’Kwa mfano kama leo hii, asasi za kiraia zimeungana katika kuitisha kongamano hili, ambalo kila mmoja atatoa maoni yake, na huwenda sulhu ya pamoja, ikapatikana,’’alieleza.

Mwenyikiti wa kamati ya kuelekea siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji Nassor Bilali Ali, alisema lazima jamii ikae chini na kufikiria upya, suala la kuwa na malezi ya ushirikiano.

Alieleza kuwa, kama yapo mambo jamii wanashirikiana mfano harusi, msiba na hivyo hivyo utamaduni huo uhamishiwe kwenye malezi ya pamoja.



Mwakilishi kutoka wizara ya Jinsia, Wazee, Maendeleo ya wanawake na watoto Pemba, Omar Mohamed Ali, alisema wizara pekee ni vigumu, kumaliza vitendo hivyo.

‘’Sisi tupo kama kutoa miongozo, sera na maelekezo kwenye mapambano dhidi ya udhalilishaji, sasa lazima na wengine tushirikiane katika kuona, hili linafikia pahala pazuri,’’alieleza.

Mapema akiwasilisha utafiti wa kihabari wa mapambano dhidi ya udhalilishaji, uliofanywa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania ‘TAMWA-Zanzibar’ mwanaharakati Safia Saleh Sultan, alisema utafiti umegundua kuwa wapo baba wazazi 13, waliowabaka watoto wao wa kuwazaa.

Aidha utafiti huo umeibua, baba walezi 25, Unguja wakiwa 13 na na Pemba 12, ambao nao wamewabaka watoto wao walezi, na kutumia nafasi yao vibaya.




Hata hivyo mwanaharakati huyo alisema kuwa, wapo waalimu wa madrasa 20, Unguja na Pemba, waliotuhumiwa kuwadhalilishaji wanafunzi wao.

Wakichangia kwenye kongamano hilo, washiriki hao akiwemo sheikh Abdalla Nassor Mauli, alilipongeza Jeshi la Polisi, kwa kubadilika katika utendaji wao wa kazi.






Nae Fatma Maulid Kassim kutoka kituo cha mkono kwa mkono wilaya ya Chake chake, alipendekeza kuwa, kama wapo wazazi, walezi na watu wengine wanakataa kutoa ushahidi, sheria ichukue nafasi yake.

‘’Hiwezekani serikali na wanaharakati hawalali usiku na mchana katika mapambano ya ukatili na udhalilishaji, kisha mwengine anaejua kila jambo, ashindwe kuvisaidia vyombo vya sheria,’’alieleza.

Nae mjumbe wa sheha kutoka shehia ya Vitongoji Fatma Mohamed Ali na mwenzake Rizik Hamad Ali, walisema kama kuna madaktari au watendaji wa Jeshi la Polisi, wanavizisha kesi hizo, wachukuliwe hatua.






Hata hivyo mjumbe wa kamati hiyo Khalfan Amour Mohamed, alisema mporoko wa maadili, rushwa muhali na wazazi kukubali kuzimaliza kesi hizo nje ya mahakama, yanachangia kuendelea kuweko.






Kongamano hilo, ni sehemu ya shamra shamra za kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, ambapo makongamano kama hayo yamefanyika wilaya zote za Pemba.

                                         Mwisho     

 

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’