MKURUGENZI 'CHAPO' AWAVUTIA PUMZI WAJUMBE WATORO WA VIKAO

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA:::

MKURUGENZI wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya watendaji wa jumuiya hiyo, kukumbwa na dharura kila panapoitishwa vikao.

 

Alisema, wapo baadhi ya watendaji sasa wamekuwa ndio ugonjwa wao usio na tiba wa kutohudhuria vikao, jambo ambalo kwa baadhi ya wakati, hurejesha nyuma mipango na mikakati yao.

 

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo, Novemba 5, mwaka 2022, ofisini kwake mjini Chake chake, wakati akizungumza na watendaji wake, kwenye kikao cha robo ya nne ya mwaka.

 

Alisema vikao ni sehemu muhimu ya kutengeneza, kuunda au kuamua jambo husika kwa maslahi ya wananchi wa wilaya ya Chake chake, sasa ikiwa kuna wajumbe ni wagonjwa kwa dharura wanaweza kukwamisha jitahada.

 

Alisema kuanzia sasa ‘CHAPO’ itakuwa wakali kwa wajumbe watoro na wasiopenda kufuata wakati wa vikao husika, kwani kinyume chake, wanaweza kukwamisha baadhi ya mambo.

 


Alieleza kuwa, inafamika kuwa kila mmoja anayotaasisi anayoifanyia kazi, lakini haina maana kuwa, wanapokuwa na shughuli zao, iwe vigumu wengine kuhudhuria.

 

‘’Ni kweli ndani ya wasaidizi wa sheria, tunao ambao ni watumishi wa umma, lakini tukumbuke tumebeba mazingo wa jamii wa kuwahudumia kisheria,’’alieleza.

 

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo, aliwasilisha yatokanayo na mkutano uliofanyika Dodoma hivi karibuni, chini ya ufadhili wa mfuko huru wa msaada wa kisheria ‘LSF’ ambao umesisitiza uwajibikaji.

 

’Kutakuwa na ufuatiliaji wa taasisi yetu na hata msaidizi wa sheria mmoja mmoja katika jimbo, shehia na kijiji, ili wanaofanya ufuatiliaji na tathmini, wajiridhishe.

 


Nae Mratibu wa Jumuiya hiyo Mohamed Hassan Abdalla, alisema ni vyema kila mmoja, kuanza kujipanga upya katika utendaji wake wa kazi, ili kuona ‘CHAPO’ inazidi kupata heshima kwa jamii.

 

‘’Sisi kwa Zanzibar ndio jumuia ya pili kutuma ripoti ya mwaka, sasa lazima tujipange, tushirikiane na tusaidiane, ili ubora na utendaji wetu upande juu,’’alieleza.

 

Msaidizi Mratibu wa ‘CHAPO’ Khadija Said Khalfan, alisema ni vyema kwa wanaopata mafunzo, kuhakikisha wanaporudi wanawawezesha na wenzao.

 


‘’Haiwezekani mtu anakwenda mafunzo akirudi anayaweka kapuni, na kama tukiendelea na utamaduni huu, itakuwa ndani ya CHAPO wataalamu ni kidogo,’’alishauri.

 

Nao wasaidizi wa sheria wa Jimbo la Chake chake Abeda Said na Mashavu Juma Mabroku, walisema lazima mkazo uwekwe wa kuendelea kushirikiana kama zamani, wakati wa utoaji wa elimu ya kisheria vijijini.

 

Kwa upande wake mshika fedha wa CHAPO Riziki Hamad Ali, alisisitiza suala la ulipaji wa ada na michango kwa wale wanaopata mikutano kupitia Jumuiya hiyo.

 




Katika kikao hicho cha robo ya mwisho wa mwaka, wasaidizi wapya wa sheria watano, wametakiwa kuwa karibu na wasaidizi waliowatangulia ili kupata uwelewa.

 

Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba, ‘CHAPO’ ambayo shughuli zake kuu ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya malipo, inawahudumia wananchi wa shehia 32 zilizomo kwenye majimbo ya Chake chake, Wawi, Ole, Chonga na Ziwani.

               Mwisho   

 

 

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’