WANANCHI DODO PEMBA WAIPA TANO CHAPO

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI wa shehia ya Dodo wilaya ya Mkoani Pemba, wameipongeza Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ kwa uamuzi wake wa kuwafuata na kuwape elimu ya umuhimu wa upimaji wa ardhi zao, ambao unaweza kuwa suluhu ya migogoro.

Walisema zipo tasisi kadhaa, zimaekuwa zikijifungia ndani na kukaa na wataalamu wao ofisini, huku wananchi wakikosa uwelewa wa mambo kadhaa, ingawa kwa ‘CHAPO’ wao hilo hawakulibali.

Wakizungumza kwenye mkutano wa wazi, ulioandaliwa na ‘CHAPO’ kwa kushirikiana na ‘the foundation for civil Society na Search for Common Ground’ na kufanyika August 4, 2022 skuli ya Dodo, walisema uamuzi huo, unafaa kuungwa mkono.

Wananachi hao walisema, elimu ya njia ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani, umuhimu wa kusajili ardhi, utambuzi wa mipaka na kuitumia Kamisheni ya wakfu kwenye urithi, ni mambo mema kwao.

Mmoja kati ya wananchi hao, Faki Shaib, alisema CHAPO imefanya jambo jema, na wameona umuhimu wa kuhudhuria mkutano huo.

‘’Kama elimu hii ya umuhimu wa usajili wa radhi, nini maana ya ardhi kisheria, njia za kumiliki ardhi na urithishaji kwa kutumia Kamisheni ya wakfu, twengeipata zamani, kusingekweko migogoro ya ardhi,’’alieleza.


Nae Seif Ali Seif alieleza kuwa, wafadhili wa CHAPO waliowawezesha kuwafikia wao Dodo, hawakukosea uamuzi huo, na wanafurahia mano ujio wao.

Kwa upande wake mwananchi Ali Juma Abdalla, alieleza kuwa awali walikuwa na hofu ya kuzifikisha ardhi zao Idara ya upimaji, wakihofia gharama kubwa.

Aidha alieleza kuwa, walikuwa hawajui kuwa, kwa sasa gharama za urithishaji kutoka Kamisheni ya wakfu serikali imeshapunguza.

‘’Mkutano huu wa leo, mimi umenitoa kwenye giza na sasa naishi kwenye mwanga, kuhusu umuhimu wa kuzitumia idara za serikali, katika urithishaji au ununuzi wa ardhi,’’alieleza.

Mapema Mkurugenzi wa, ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, amesema pamoja na uwepo wa wasaidizi wa sheria, lakini wameamua kuwafuta wananchi hao.

Alieleza kuwa, lengo la mkutano huo ni kuwaelekeza wananchi athari za kila mgogoro wa ardhi kuupeleka mahakamani, ambapo kwanza watapoteza gharama na suluhu itakuwa ngumu.

‘’Endeleeni kuitika wito kila mnaposikia uwepo wa mikutano, maana faida zake ni kubwa, na leo hii naamini baada ya kuwasikiliza wataalamu, mmeelewa chanzo cha migogoro ya ardhi,’’alifafanua.

Kwa upande wake mwakilishi wa the foundation for Civil Society Georgina Lund, amesema wanaendesha mradi mkubwa wa dumisha amani Zanzibar, ambao sasa unatimiza miezi 18.

Mwakilishi huyo, alieleza kuwa moja ya eneo ya utekelezaji wa mradi huo, ni kuwaelekeza wananchi namna bora ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani.

Alieleza kuwa, ardhi imekuwa tishio kubwa la uwepo wa migogoro ndio, maana jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’, imeamuwa kuwaelekeza wananchi.





Akizungumza na wananchi hao, Mratibu wa Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba, Safia Saleh Sultan, alisema, makosa yote ya madai, ni vyema jamii wakayawekea vikao vya familia.

‘’Ni makosa ya madai pekee na sio jinai, ambayo jamii wanaweza kukaa na kuyafanyia sulhu, na wala sio busara kuyapeleka mahakamani, maana changamoto zake ni kubwa, ikiwemo gharama,’’alieleza.






Afisa Utambuzi wa Ardhi Pemba Faki Ali, amesema ardhi iliyotambuliwa na kupatikana hati ya matumizi, huongeza thamani yake.

Hata hivyo amewakumbusha wananchi kuwa, kuanza sasa mpango wa utambuzi wa ardhi zao, na sio kusuburi ule wa serikali, ambao umeshaanza katika baadhi ya shehia.



Akighairisha mkutano huo, sheha wa shehia ya Dodo Ramadhan Far-han Far-jala, ameipongeza CHAPO, kwa kuamua kuwafuata na kuwapa elimu hiyo.

Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ambayo imeanzishwa mwaka 2016, kwa sasa inaendelea na mradi ‘Kujenga uwelewa kwa jamii, katika kuzuia migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi katika shehi za Dodo, Pujini na Mfikiwa Mkoa wa kusini Pemba.

                      Mwisho       

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’