CHAPO: WANANCHI CHAKE CHAKE ENDELEENI KUSHIRIKI ZOEZI LA SENSA
NA HAJI NASSOR, PEMBA
JUMUIYA ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chakechake 'CHAPO' imewakumbusha wananchi wilayani humo, kuendelea kushirikiana na makarani wa sensa, ili kufanikisha zoezi hilo.
Wito huo umetolewa leo August 25, mwaka 2022 na Mkurugenzi wa 'CHAPO' Nassor Bilali Ali wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, juu kuelekea zoezi linaloendelea la sensa ya watu na makaazi.
Alisema ni vyema kwa wananchi kuhakikisha wanaandaa na kupanga shughuli zao vizuri, ili makarani wa sensa watakopfika kutaka taarifa iwe rahisi kupatikana.
Mkurugenzi huyo alisema zoezi hilo huja kila baada ya miaka 10, hivyo ni wajibu kwa wananchi kufurahia na kushiriki vyema, ili serikali iweke mipango na mikakati yake vyema vya maendeleo.
"Wananchi wa wilaya ya Chakechake tunawaomba kuwa tayari zoezi hilo la sensa limeshaanza tokea August 23, mwaka huu, hivyo ni wajibu kwao kushirikiana na masensa pale watakapofika kwenye maeneo yao kwa kuhesabiwa,"alisema.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa CHAPO, amewataka wananchi hao wa wilaya ya Chakechake kwa wale ambao watakuwa na dharura wakumbuke kuacha taarifa rasmi majumbani, ili iwe rahisi kwa makarani.
Alifafanua kuwa, moja ya viambatanisho ni vitambulisho husika ili kuwasaidia makarani kupata taarifa kwa kina.
Hata hivyo amewakumbusha wananchi hao kuto taarifa za ukweli kwa makarani hao, ambazo hizo zitasaidia katika kupatikana kwa kweli zitakazosaidia kwa taifa.
"Taarifa hizo zitakuwa ni siri baina ya makarani na mtoa taarifa, hivyo ni vyema wakalijua hilo,"alifafanua.
Nae mtendaji wa CHAPO Mohamed Hassan alisema zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo ni kosa kulikwepa.
Kwa upande wake Mratibu wa miradi kutoka 'CHAPO' Siti Hamad Ali amewakumbusha wazazi na walezi kutowaficha watoto wao wenye ulemavu.
"Hata watoto wenye ulemavu wanatakiwa nao wahesabiwe hivyo, hakuna haja ya kuwaficha maana nao wanatakiwa taarifa zao zipatikane,"alifafanua.
Hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Chakechake Abdalla Rashid Ali amewataka makarani wa sensa kutumia lugha nzuri wakati wanapowahudumia wananchi..
Zoezi la sensa la watu na makaazi ambalo hufanyika kila baada ya miaka 10, limerejea tena August 23 mwaka 2022 baada ya kumalizika la mwisho mwaka 2012.
Mwisho


Comments
Post a Comment