WANANCHI PUJINI WATAJA VYANZO VYA MIGOGORO YA ARDHI
NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WANANCHI wa shehia za Pujini, Mfikiwa na Dodo
mkoa wa kusini Pemba, wamesema moja ya sababu inayochangia uwepo wa migogoro ya
ardhi katika jamii, ni ucheleweshwaji wa mirathi kwa wahusika.
Walisema, wapo baadhi ya wanaume katika
familia, mara baada ya kifo cha mrithiwa, huikumbatia mirathi na wakati
mwengine hadi kuwapa lugha za vitisho warithi wenzao, na mwisho huzaliwa
migogoro inayozuilika.
Wakichangia mada ya usuluhishi wa
migogoro ya aradhi, kwenye mafunzo ya kuzuia migogoro kwenye maeneo ya uwekezaji
na kufanyika kituo cha ubunifu wa kisayansi Pujini, wananchi hao walisema, hilo
bado ni tatizo.
Walieleza kuwa, wanaume hao wamekuwa
wakipuuzia maandikiko matakatifu yanayohimiza suala la kulipa kipaumbele
urithi, mara baada ya muhusika kufariki.
Mmoja kati ya wananchi hao Abdallah
Kombo, alisema utamaduni wa kumilikiwa mirathi na mtu mmoja, na kuwaacha
wengine pembeni, huzaa migogoro mfano kama ya ardhi.
‘’Moja ya sababu ya uwepo wa migogoro
na hasa ya ardhi, ni wanaume kutokubali kurithi kwa haraka, na kisha huamua
kutumia wao na watoto wao na kuwaacha wengine kama vile hawana haki,’’alieleza.
Nae Khamis Rashid Khamis, alisema
utamaduni huo huwaathiri zaidi wanawake na hasa kwa vile wakati mwengine,
huwekewa vitisho na kaka au ndugu zao.
Nao wananchi Subira Khami Juma, Asha
Faki Juma na Nassra Bakar Seif, walisema jambo jengine linapolekea uwepo wa
migogoro ya ardhi, ni tamaa ya baadhi ya watu.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo
hayo, Afisa Programu kutoka taasisi ya Foundation for Civil Society ‘FCS’ ya
Tanzania bara, Eveline Mchau, alisema
Zanzibar inakabiliwa na migogoro kadhaa, ingawa ya ardhi yako juu.
Alisema FCS, imekuwa ikifadhili
mashirika kadhaa ili kuona, sasa jamii inabuni mbinu ya kuhakikisha kunawepo na
njia za amani na usuluhishi, ambazo hazitojenga chuki miongoni mwao.
Alisema uwezeshaji wao wa sasa yapo
mashirika zaidi ya tisa, yakiendelea na mradi huo, moja wapo ni Jumuiya ya
wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake 'CHAPO' ambao wanaendelea kukutana na
wadau.
‘’Niwapongeze wenzetu wa ‘CHAPO’ kwa
kuendelea na mradi huu, na yapo mashirika mengine yanaendelea kutekeleza mradi
mkubwa wa dumisha amani Zanzibar, ambao pia umezaa mradi wa kujengea uwezo
jamii wa kuzuia migogoro ya ardhi katika uwekezaji,’’alifafanua.
Mkurugenzi wa CHAPO Nassor Bilali Ali, aliwakumbusha wananchi kuwa, migogoro ya ardhi katika maeneo ya uwekezaji yanazuilika, ikiwa jamii itafuata taratibu za umiliki wa aradhi.
Alieleza kuwa, wapo wananachi wamekuwa
wakitumia ardhi bila ya kuwa na nyaraka za umiliki wala matumizi, na
wanapotokezea wamiliki halali, ndio huwa chanzo cha migogoro.
Akiwasilisha mada ya utatuzi wa
migogoro ya ardhi, Mwanasheria kutoka Kamisheni ya ardhi ‘COLA’ kisiwani Pemba
Asha Suleiman Said, alisema zipo njia tano halali za umiliki wa ardhi.
‘’Moja wapo ni kununua, kupewa kama
zawadi, kupimiwa na serikali, kurithi pamoja na kuomba serikalini, ambapo njia
zote hizo kisha hufuatwa na nyaraka halali, ili kuepusha migogoro,’’alifafanua.
Kwa upande wake mwanasheria Khalfan
Amour Mohamed, wakati akiwasilisha mada ya njia za uwekezaji, alisema hata
mwananchi wa kwaida, anaweza kutoa ardhi yake.
‘’Kisheria ukishaitoa ardhi kwa mwekezaji
na akishindwa kuendeleza mradi aliokusudia, serikali itaichukua na kutafutwa kwa
mwekezaji mwengine, na hairudi moja kwa moja kwa mmiliki wa awali,’’alifafanua.
Mapema Mratibu wa mradi wa kuwajengea
uwezo wananchi kuzuia migogoro kwenye maeneo ya uwekezaji kutoka ‘CHAPO’ Riziki
Hamad Ali, alisema ardhi ya Zanzibar haiuzwi kwa mgeni bali hukodishwa.
‘’Kupitia mradi huu wa mwezi mmoja,
tunakusudia pia kuanzisha kwa kwa baraza ya usuluhishi ya migogoro ya ardhi,
maana sio kila mgogoro unapelekwa mahakamani,’’alieleza.
Hata hivyo amewakumbusha masheha
kuwachagua wajumbe wa kamati za usuluhishi wa migogoro, wenye uwezo wa
kushauri, wanaokubalika na wenye uwelewa wa mipaka na umiliki wa ardhi.
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ ambayo
imeanzishwa mwaka 2016, moja ya majukumu yake ni kutoa elimu, ushauri na msaada
wa kisheria bila ya malipo.
Jumuiya hiyo kwa sasa inaendesha mradi wa mwezi mmoja wa kuijengea uwezo jamii, kuzuia migogoro katika ardhi ya uwekezaji, ukitekelezwa shehia za Pujini, Dodo na Mfikiwa ukifadhiliwa na the foundation for civil society kwa muda wa mwezi mmoja.
Mwisho




.jpg)
.jpg)











Comments
Post a Comment