RC KUSINI PEMBA: AIPONGEZA KAMATI MAANDALIZI SIKU YA MTOTO AFRIKA -PEMBA

  


NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-

MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema ameridhishwa na matayarisho ya awali, yaliyofanywa na wajumbe wa Kamati maalum ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika, kisiwani humo.

Alisema, kamati hiyo imeibua jambo kubwa la kutaka kufanya maadhimisho hayo, na kujipanga kwa kufanya shughuli mbali mbali, kabla na wakati wa kilele chenyewe ambacho ni Juni 16, mwaka huu.

Alisema ameridhishwa na mpango huo wa maadhimisho na kuahidi kushirikiana nao, hadi kukamilika kwake siku ya kilele hicho kinachotarajiwa kufanyika uwanja wa Gombani.

Mkuu huyo wa mkoa aliyasema hayo Juni 11, 2022 ofisini kwake Chake chake, wakati akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, waliofika ofisini kwake, kuwasilisha mpango pendekezwa wa kilele hicho.

Alisema, suala la kuwashirikisha watoto ambao ni wanafunzi na kuwaandalia michezo mbali mbali kama ushindani kwenye elimu, ni jambo linalofaa kuungwa mkono.

‘’Kwanza niwapongeze wajumbe wa kamati hii, kwa uamuzi wao wa kutaka kushirikiana na kuiunga mkono serikali yetu, katika kutetea na kulinda haki za mtoto,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa, aliitaka kamati hiyo, wawasiliana nae kila wakati, na ikiwa kuna jambo limekwa, kuona njia gani ya kulitatua.

‘’Kwenye usafiri, majukwaa na hata kikundi cha brass band na gharama nyingine, nitaangalia uwezekano wa kushirikiana na wenzangu kuzitekeleza,’’alifafanua.

Mwenyekiti wa muda wa kamati hiyo Nassor Bilali Ali, alimpongeza mkuu huyo wa mkoa, kwa uamuzi wake, wa kuzibeba gharama za utekelezaji wa sherehe hizo.

‘’Kwa niaba ya wajumbe wa kamati, tunakupongeza kwa hatua zako na kuona sherehe hii ya kutetea haki za mtoto zinafanyika kwa ufanisi,’’alieleza.

Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, Mwanaisha Ali Massoud, alisema mfano wa viongozi kama Mkuu wa mkoa, ndio ambao wanaweza kufanikisha mambo kadhaa.

‘’Kwa hakika ilionekana dhahiri tumeshakwa kuiadhimisha siku hii, lakini kutokana na umahiri, utayari na kuumwa kwake na haki za watoto, ndio maana ameamua kusaidia eneo kubwa,’’alieleza.

Wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Siti Habib Mohamed kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, alisema watoto lazima waandaliwe zawadi maalum.

‘’Kwa vile tumeamua kuweka michezo kama ya kuokota mbatata, kuvuta kamba, mbio za magunia, masuali ya papo kwa papo, ni vyema washindi wakatunzwa,’’alipendekeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba TUJIPE, Tatu Abdalla Msellem, alisema moja ya changamoto zinawazowakabili watoto, ni janga la udhalilishaji.

‘’Hivyo kama tumepanga tutakua na masuali ya papo kwa papo, basi hata kuwauliza nini maana ya udhalilishaji, hatua gani utazichukua ukimkuta aliyedhalilisha na mengine yanayofanana na hayo,’’alishauri.

Awali Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, aliitaka kamati hiyo, kuyafanya maadhimisho hayo kuwa ya kitaifa kisiwani Pemba badala ya kuadhimishwa kiwilaya.

Kamati hiyo inaundwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria Pemba ‘JUWASPE, Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba TUJIPE, na Zanzibar Social Workers Association ZASWA.

                           MWISHO   

AA

Comments

Popular posts from this blog

AFISI YA MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR YAKUSANYA MAONI SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

MKURUGENZI HANIFA, AWAUMA SIKIO WANANCHI WAWI HAKI ZA BINAADAMU

‘WANANCHI HAWANA MAMLAKA YA KUONDOSHA UHAI WA MTU’