MKURUGENZI CHAPO AWAKARIBISHA WASAIDIZI WA SHERIA WAPYA CHAKE CHAKE
NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
MKURUGENZI wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake 'CHAPO' Nassor Bilali Ali, amewataka wasaidizi wa sheria wapya, wa majimbo ya wilaya hiyo, kufanyakazi kwa bidi, ili kuisaidia jamii, kupunguza matendo ya udhalilishaji.
Alisema, jamii inakabiliwa na majanga kadhaa pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya, migogoro ya ndoa, ardhi na matunzo ya watoto, hivyo ni wajibu wao kuona hayo yanapungua.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, baada ya kuwapokea wasaidizi hao wa sheria, alisema amefarajika kuona, Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, imewapa mafunzo vijana hao.
Alisema, moja ya eneo la Zanzibar ambalo haliko salama na majanga mbali mbali ni wilaya ya Chake chake, hivyo wasaidizi hao wa sheria, wanayokazi ya kufanya ndani ya jamii.
‘’Karibuni sana kwenye jumuiya yetu hii, na sisi tumefarajika kuona, tumepata damu changa ya kupambana na majanga mbali mbali, ili tuwe na taifa lenye amani,’’alieleza.
Aidha Mkurugenzi huyo, alisema wakati wa utendaji wao kazi watakuwa karibu na wenzao waliowatangulia, hivyo ni jukumu lao, kuwashirikisha katika harakati zao.
Katika hatua nyingine, alisema kazi iliyofanywa na Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kupitia Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, ya kuwa na mradi wa kuimarisha upatikanaji haki Zanzibar, ni jambo jema.
‘’Kupatikana kwa wasaidizi wa sheria 50 Unguja na Pemba na wale watano wa majimbo ya wilaya ya Chake chake, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo,’’alieleza.
Hata hivyo, amewakumbusha wasaidizi hao wa sheria, kujiendeleza kielimu zaidi, ili hapo baadae wawe wanasheria kamili.
Nao wasaidizi hao wa sheria, walisema walikuwa na hamu kubwa ya kupata mafunzo hayo, na sasa kilichobakia mbele yao ni kuihudumia jamii.
Mtarajiwa msaidizi wa sheria Jimbo la Ziwani Nassra Bakar, alisema anachoomba ni ushirikiano wa karibu na wasaidizi wa sheria wakongwe, ili kufanikisha ndoto zake.
Kwa upande wake mtarajiwa msaidizi wa sheri Jimbo la Ole Tuheni Talibu, alimuomba Mkurugenzi huyo, kuangalia uwezekano, wa kuandaa mikutano katika majimbo yote.
Nae mtarajiwa msaidizi wa sheria Jimbo la Chake chake Wahid Kombo, alisema kazi anayoiona ya kuanza nayo, ni kukutana na wanafunzi wa madrassa, ili kuwapa elimu ya kujikinga na matendo ya udhalilishaji.
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ iliyopo mkabala na Tume za Uchaguzi Chake chake, ambayo imeanzishwa mwaka 2016, moja ya malengo yake ni kuisaidia jamii kufikia upatikanaji wa haki, elimu, ushauri na msaada wa kisheria kwa maskini na watu wenye ulemavu bila ya malipo.
Mwezi Mei mwaka huu, jumla ya wasaidizi wa sheria 18 wa mjimbo ya uchaguzi ya Pemba, waliungana na wenzao 32 wa majimbo ya Unguja, kupata mafunzo ya awali ya wasaidizi wa sheria, yalioendeshwa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kwa ufadhili wa LSF.
MWISHO



Comments
Post a Comment